Abstract:
Matini za kishairi ni miongoni mwa matini ambazo zimesemekana kuwa tata kutafsiriwa kwa ufasaha. Utafiti huu ulijikita katika kuchunguza changamoto za kutafsiri ushairi wa: Wimbo wa Lawino wa Paul Sozigwa (1975). Utafiti huu ulinuia kuchunguza sababu zilizopelekea kuwe na changamoto za kiisimu katika ushairi mfano wa: Wimbo wa Lawino wa Paul Sozigwa. Kadhalika, tulichunguza jinsi changamoto hizi za kiisimu ziliathiri matumizi ya lugha, hivyo kupelekea kuwe na athari katika ujumi. Nadharia zilizotumiwa zilikuwa niza kiisimu na kimawasiliano.Muundo wa utafiti ulikuwa ni uchanganuzi wa kiuthamano. Mtafiti alichunguza mashairi kumi na tatu huku akiangazia masuala ya kiisimu, matumizi ya lugha na ujumi.Matini chanzi ilikuwa kitabu cha Kiingereza: Song of Lawino cha Okot P’ Bitek aliyeandika Wer Pa Lawino katika lugha ya Kiacholi. Matini lengwa ilikuwa kitabu cha Kiswahili: Wimbo wa Lawino cha Paul Sozigwa. Matokeo yalionyesha kuwa kwa kiasi fulani mtafsiri aliweza kudumisha umbo la shairi la matini chanzi ambao ulikuwa huru. Hata hivyo hakufaulu kudumisha miundo ya beti na mishororo kwa sababu za utofauti wa mifumo katika lugha mbili, kutotafsiri baadhi za istilahi, kutafsiri kupita kiasi cha haja na kutotafsiri kikamilifu baadhi ya istilahi zilizotumiwa katika matini chanzi.